Polisi mjini Hong Kong leo imevamia ofisi za tovuti moja ya habari za mtandaoni inayounga mkono demokrasia baada ya kuwakamata watu sita kwa njama ya kuchapisha chapisho la uchochezi, hii ikiwa hatua ya hivi karibuni zaidi ya ukandamizaji dhidi ya upinzani mjini humo.
Wale waliokamatwa wanahusishwa na kituo cha habari cha Stand News ambacho ni moja kati ya vituo vinavyounga mkono demokrasia mjini humo baada ya gazeti la Apple Daily ambalo pia lilikuwa likiunga mkono demokrasia kuacha kufanya kazi mapema mwaka huu.
Waliokamatwa wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka miwili jela na faini ya hadi dola 640.Polisi inasema kuwa zaidi ya maofisa wake 200 walihusika katika msako huo na kwamba walikuwa na kibali cha kukamata vifaa muhimu vya uandishi wa habari chini ya sheria ya usalama wa kitaifa iliyopitishwa mwaka jana.
