
Watu wawili mama na mwanawe wamehukumiwa kifungo cha miaka 40 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la uhujumu uchumi.
Hakimu mkazi Mfawidhi, Robert Kaanmwa, wa mahakama ya wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu, aliwatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja, Kija Matu (60), na Mayunga Juma (30), baada ya kukiri kukutwa na nyama ya nyumbu kinyume cha sheria.
Mahakama iliambiwa washtakiwa walikutwa na nyara hiyo ya serikali Desemba 5, 2022, saa 4:00 usiku, katika kijiji cha Laini ‘B’, wilaya ya Itilima, mkoa wa Simiyu.
Hati ya mashtaka ilidai kuwa washtakiwa hao walikutwa na vipande vinane vya nyama ya nyumbu kinyume cha sheria, vikiwa na thamani ya sh. milioni 1,517,100.
Kesi hiyo No. 1 ya mwaka 2022 ya uhujumu uchumi, kabla ya hukumu hiyo kutolewa washtakiwa walisomewa mashtaka yao na Mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi, kutoka ofisi ya mashtaka, Jaston Haule. Hiyo ni kesi ya kwanza kutolewa hukumu tangu mahakama hiyo izinduliwe rasmi Novemba 25, 2022 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahimu Juma.
