Mwigizaji mkongwe wa India, Nana Patekar, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75 baada ya kupata mshtuko wa moyo katika makazi yake Dona Paula, Goa, Alhamisi Oktoba 8, 2026. Taarifa kutoka Manipal Hospital zimeeleza kuwa alifikishwa hospitalini akiwa tayari hana fahamu, huku madaktari wakithibitisha kifo chake baada ya juhudi za kumuokoa.
Kwa mujibu wa daktari Shekhar Salkar wa Manipal Hospital, Patekar alikuwa ametuma ujumbe kwa rafiki yake majira ya saa 2:30 usiku akieleza kuwa alikuwa hajisikii vizuri na alikuwa na maumivu upande wa kushoto. Rafiki huyo aliona ujumbe huo baadaye na kufika nyumbani kwake majira ya saa 4:00 asubuhi, ambapo alimkuta akihema kwa shida na kutokwa jasho.
Timu ya matibabu ilifika katika makazi yake na kuanza kumpa huduma ya CPR kabla ya kumpeleka hospitalini, huku juhudi hizo zikiendelea njiani na hospitalini. Madaktari waliendelea na CPR kwa takribani dakika 45 hadi saa moja, lakini hawakuweza kumuokoa, na alitangazwa kuwa amefariki saa 5:20 asubuhi. Mwili wake ulipelekwa Goa Medical College kwa uchunguzi wa kitabibu ili kubaini kwa kina chanzo cha mshtuko huo wa moyo.
Patekar alikuwa miongoni mwa waigizaji waliokuwa na ushawishi mkubwa katika sinema za Kihindi na Kimarathi, akiwa na kazi iliyodumu kwa takribani miongo mitano. Alianza katika filamu mwaka 1978 na baadaye akapata umaarufu kupitia kazi kama Parinda Krantiveer, Prahaar na Salaam Bombay, huku akijulikana kwa uigizaji wenye nguvu na uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali.
Katika maisha yake ya kisanii, Patekar alishinda Tuzo tatu za National Film Awards na kutunukiwa Padma Shri, moja ya heshima kubwa za kiraia nchini India. Mbali na uigizaji, pia alifanya kazi kama mwongozaji na mtayarishaji wa filamu, huku mchango wake katika masuala ya kijamii ukiwemo ushiriki wake katika Naam Foundation, iliyolenga kusaidia wakulima na juhudi za uhifadhi wa maji.
Kifo cha Patekar kimeibua maombolezo kutoka kwa viongozi na wasanii nchini India, akiwemo Waziri Mkuu Narendra Modi, aliyemsifu kwa umahiri, upekee na uwezo wa kuacha alama katika kila nafasi aliyocheza. Muigizaji Akshay Kumar pia ametoa salamu za rambirambi, huku Patekar akiacha nyuma mke wake na mtoto mmoja wa kiume.
