*Mtoto kupigwa na baba
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mgeule, kata Buyuni, manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam, John Mwatebela, amesema si vema wazazi kutoa adhabu kwa watoto wao wakati wakiwa na hasira kwani wanaweza kuwaumiza.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake waliotaka kufahamu tukio la mkazi wa mtaa huo, Erick Kigala, kumwadhibu kwa kumpiga kwa waya hadi kumtoa utumbo nje binti yake mwenye umri wa miaka Saba(jina limehifadhiwa).
Erick alimwadhibu binti yake huyo kwa kosa la kuto sahihisha daftari zake shuleni muda wa wiki nzima.
“Ni kweli tukio hili lilitokea na mtoto alishapelekwa hospitali, sasa anaendelea vizuri. Nitoe mwito kwa wazazi ambao ndiyo walimu wa kwanza wa mtoto wanapotoa adhabu kwa lengo la kumwonya wazingatie umri wake.
Baba wa mtoto huyo Erick Kigala, amesema anajutia kosa hilo na kwamba hatarudia tena.
“Mimi ni baba wa watoto wanne, nimewalea katika kipindi cha zaidi ya miaka 10, sikuwahi kufanya kosa kama hili, lengo langu lilikuwa kusimamia maadili mema kwa mtoto wangu na wala sikujua kama linaweza kutokea hili.
“Ndiyo maana nilimpeleka mwanangu hospitali ambapo nimebaini kuwa mtu ukizaa sio wako peke yako, bali ni wajamii nzima, kwani vyombo vya dola vilifuatilia na kulisimamia jambo hili, kwa nguvu zote,” amesema.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Tusekile Kiamba amesema ana amini tukio hilo lilitokea kwa bahati mbaya tu kwa sababu mumewe ni baba mzuri kwa watoto wao.
