Msichana mwenye umri wa miaka 15, Yuleidy Ixcotoyac, ameripotiwa kupata fahamu akiwa ndani ya jeneza wakati familia yake ikiomboleza kifo chake katika Kijiji cha El Jocote, Wilaya ya Sacapulas, Mkoa wa Quiché nchini Guatemala, Oktoba 10, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini humo, msichana huyo alipoteza fahamu alfajiri baada ya kulalamika maumivu makali kifuani wakati baba yake, Abraham Ixcotoyac, alipokuwa akimpeleka kwenye kituo cha afya kwa ajili ya matibabu.
Baba yake amesema walipokuwa njiani kuelekea hospitalini, alibaini kuwa binti yake hakuwa akipumua na hakuhisi mapigo ya moyo wake. Hata hivyo, msichana huyo hakufikishwa hospitalini wala kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu kuthibitisha hali yake.
Baada ya kudhani kuwa amefariki dunia, baba yake alitafuta huduma za kampuni ya mazishi ili kupata jeneza na kumrudisha nyumbani, ambako ndugu, majirani na waumini wa kanisa lao walikusanyika kwa ajili ya shughuli za kuomboleza.
Mama wa msichana huyo, Lesvia Ríos, amesema hakuwa amepoteza matumaini kuwa binti yake alikuwa hai. Alieleza kuwa alipokuwa karibu na jeneza huku akilia, aliona mwili wa binti yake ukisogea.
Muda mfupi baadaye, watu waliokuwa kwenye eneo hilo walisikia kelele na walipofika karibu na jeneza, walimkuta msichana huyo akianza kupata fahamu na kuinuka. Video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha watu wakimsaidia kutoka ndani ya jeneza na kumpa maji.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Yuleidy alisema alianza kusikia maumivu makali kifuani kabla ya kupoteza fahamu, akieleza kuwa kifua chake kilihisi kizito.
Msichana huyo alitoa shukrani kwa wazazi wake na watu waliowafariji, akieleza tukio hilo kuwa muujiza katika maisha yake.
Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na mamlaka za afya nchini Guatemala kueleza kilichosababisha msichana huyo kupoteza fahamu na kudhaniwa kuwa amefariki dunia, kisha kupata fahamu akiwa ndani ya jeneza. Pia, hakuna maelezo ya kitabibu yaliyothibitishwa hadharani kuhusu hali yake.
