
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amefanya mazungumzo na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Dar es Salaam.
Dk Mpango ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya CCM Taifa na mlezi wa wazee mkoa wa Dar es Salaam, alifanya mazungumzo hayo jana Septemba 4, 2021 kwenye viwanja vya Karimjee.
Wakati wa mazungumzo yake amewashukuru wazee wote nchini kupitia wazee wa Dar es Salaam kwa kuendelea kutoa ushauri, malezi na kulinda mila na desturi za nchi.
Amesema mchango wa wazee nchini ni mkubwa kwani wao ndio waliopigania kuondoka kwa matabaka yaliokuwapo kipindi cha ukoloni na kusaidia kuleta uhuru wa pamoja na kuijenga nchi baada ya uhuru.
Amesema taifa litaendelea kuenzi mchango waliotoa wazee kwa wakati wote walipolitumikia na kuahidi kuendelea kutumia ushauri wao katika uongozi wake hapa nchini.
Aidha, mlezi huyo wa mkoa wa Dar es Salaam ameagiza viongozi wanaotokana na CCM kuhakikisha wanafanya ziara na kusikiliza kero za wananchi ili kuzipatia ufumbuzi wa haraka na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama hicho ya mwaka 2020.
Amewasihi wanachama wa CCM katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2022 kuwapa nafasi viongozi wenye sifa na wanaojali maslahi ya taifa ili kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema ni muhimu CCM iendelee kulinda rasilimali zilizopo ndani ya chama pamoja na kuhakikisha inajenga vyanzo vipya vya mapato na kuvisimamia.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wazee mkoa wa Dar es Salaam, Hemed Mkali, amesema wazee wanatambua juhudi zinazofanywa na serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
