
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango akitazama eneo lililotokea ajali na kusababisha vifo vya watu 19 na kujeruhi wengine 25 Agosti 16, 2022 huku nyingine ikitoke Septemba 07, 2022 ambayo ilisababisha vifo vya watu 6 katika kijiji cha Shamwengo, kata ya Inyala, mkoani Mbeya, wakati alipotembelea eneo hilo leo jana Septemba 11, 2022.

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha inakamilisha haraka barabara ya mchepukoa eneo la Mlima Inyala, kijiji cha Shamwengo, mkoani Mbeya, ili kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara katika eneo hilo.
Dk. Mpango ameyasema hayo alipotembelea eneo la Inyala mahali zilipotokea ajali mbili hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu 25.
Amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 2.5 inapaswa kujengwa kiwango cha lami haraka kama suluhisho la muda mfupi litakarorahisisha upishanaji wa magari na kukabiliana na changamoto za ajali za mara kwa mara.
Halikadhali amemwagiza Kamanda wa Polisi, mkoa wa Mbeya, Urich Matei, kuhakikisha anasimamia ukaguzi wa magari yanayopita eneo la mlima Inyala ili kuepusha madhara ya ajali zinazojitokeza kutokana na ubovu.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa siku 10 kwa Tanroads mkoa wa Mbeya kuhakikisha anamaliza ujenzi wa miundombinu ya ukaguzi wa magari inayoendelea katika eneo hilo.
Amesema serikali inasikitishwa na madhara ya ajali yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali na kuwataka wahusika wakiwamo jeshi la polisi kutimiza wajibu wao kuchukua hatua za kudhibiti ajali hizo zinazogharimu maisha ya watu.
Dk. Mpango amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha miundombinu ikiwamo upanuzi wa barabara inayopita mkoani Mbeya kuanzia Igawa hadi Tunduma mkoani Songwe.
