Polisi nchini Canada wamesema wamemkuta Damien Sanderson, mmoja wa washukiwa wa mashambulizi ya ovyoovyo ya kutumia visu, akiwa amefariki dunia.
Mwili wa Damien, aliyekuwa na umri wa miaka 31 ulipatikana karibu na eneo kulikotokea mashambulizi hayo ya visu.
Mshukiwa mwingine, kaka yake Myles Sanderson mwenye umri wa miaka 30, bado hajapatikana na polisi wanaamini kuwa ana majeraha.
Watu 10 waliuawa na 18 kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa dhidi ya jamii moja ya watu wa asili na mji ulioko karibu katika mkoa wa Saskatchewan.
Msako mkubwa ulianzishwa baada ya mauaji hayo ambayo yanatajwa kuwa mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa siku za karibuni.
Polisi imetoa waranti wa kukamatwa washukiwa hao. Maofisa wamekataa kuzungumzia chanzo cha mauaji hayo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Justin Trudeau amesema bendera itapepea nusu mlingoti kwenye jengo la bunge la Canada mjini Ottawa ili kutoa heshima kwa wahanga.
