Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mlipuko wa lori la mafuta katika Eneo la Serikali ya Mtaa ya Katcha, Jimbo la Niger, nchini Nigeria, imeongezeka na kufikia watu 42, huku zaidi ya 60 wakijeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea Jumanne, Oktoba 21, 2025, baada ya wakaazi kukimbilia kuchota mafuta kutoka lori la petroli lililopinduka kando ya Barabara ya Agaie–Bida, karibu na kijiji cha Essa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, lori hilo lililokuwa likisafirisha mafuta kutoka Lagos kuelekea kaskazini mwa Nigeria lilipinduka majira ya saa 11 alfajiri kutokana na hali mbaya ya barabara. Mafuta yalipomwagika, wakazi wa jamii za Essan na Badeggi walikusanyika na vyombo kuchota mafuta, hali iliyosababisha mlipuko mkubwa ulioharibu eneo lote.
Kamanda wa Shirikisho la Usalama Barabarani (FRSC) wa Jimbo la Niger, Hajiya Aishatu Saadu, alithibitisha awali vifo vya watu 35 na majeruhi 46, lakini taarifa mpya kutoka kwa Wakala wa Usimamizi wa Dharura wa Jimbo la Niger (NSEMA) zinaonyesha kuwa idadi ya vifo imeongezeka hadi 42 kufuatia vifo vya majeruhi waliokuwa wakipatiwa matibabu.
Majeruhi zaidi ya 60 wamepelekwa katika Kituo cha Matibabu cha Shirikisho Bida kwa ajili ya matibabu zaidi.
Tukio hili limeibua mjadala nchini humo kuhusu changamoto za miundombinu mibovu, usalama barabarani, na tabia ya hatari ya kuchota mafuta katika maeneo ya ajali. Wataalam wa usalama wameonya kuwa hali ngumu ya kiuchumi huwasukuma wananchi kupuuza tahadhari za usalama kwa tamaa ya kupata mafuta bure.
Imeelezwa, uchunguzi wa awali unaendelea kuhusu uzembe na udhibiti wa usafirishaji wa mafuta nchini humo.
