Hatimae ukweli wote umefahamika kutokana na sakata la Youssoufa Moukoko anayedaiwa kudanganya umri wake.
Ulimwengu wa soka umeingiwa na taharuki mpya inayotia shaka usahihi wa taarifa za kibinafsi za Mchezaji Youssoufa Moukoko.
Mshambuliaji huyo, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo Nice akitokea Borussia Dortmund, ameingia kwenye kashfa inayohusiana na umri wake halisi.
Mashaka yameibuka kufuatia ufichuzi kutoka kwa Joseph Moukoko, ambaye awali alitambuliwa kama babake mzazi. Joseph anadai kuwa yeye si mzazi wake wa kumzaa ila mchezaji huyo hajazaliwa Novemba 20, 2004, kama ilivyoelezwa katika nyaraka rasmi.
Badala yake, anadai kuwa mwanasoka huyo alizaliwa Julai 19, 2000, ambayo ingemfanya awe na umri wa miaka 24, badala ya miaka 20.
Idhaa ya Ujerumani ya “ProSieben” iliachia filamu ambayo Joseph Moukoko alikiri kughushi nyaraka ili kupunguza umri wa mchezaji huyo na kumtambulisha kama mwanawe. Kulingana naye, uamuzi huu ulifanywa ili kuongeza fursa za Youssoufa katika ulingo wa soka wa Ulaya wenye ushindani mkubwa.
“Tulifanya hivyo ili apate nafasi nzuri zaidi katika soka la Ulaya,” Joseph alisema.
