
CLAUDIA KAYOMBO, SINGIDA
ILI kuunga mkono mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii yaliyofikiwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili, viongozi Dini mkoani hapa, wamewataka wakuu wa idara zote serikalini kuweka mbele uadilifu na uaminifu wanapotumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali maendeleo.
Wametoa nasaha hizo jana Machi 18, 2023 wakati wa mkutano ulioandaliwa na mkuu wa mkoa huu, Peter Serukamba kubainisha mafanikio ya miaka Miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tumesikia hapa fedha zilizotolewa na Rais kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mkoa wetu (Singida), nitoe mwito kwa Idara zote wawe waadilifu katika matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Ni vizuri zitumike kulingana na taratibu, viongozi wawe waadilifu, wazipokee na kuzitumia katika unyenyekevu, waige mfano wa Rais (Mama Samia) mwenyewe mnyenyekevu na mpole wawe na huruma na upendo na watu.
“Viongozi msiishie kusema mama anaupiga mwingi, taarifa ya leo ni hatua nzuri kwa taifa letu,” alisema Sheikh Mkuu wa mkoa wa Singida, Issa Nassoro.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Syprian Hilinyi, amewataka watendaji wanaomsaidia rais mkoani hapa watekeleze miradi ya maendeleo kwa haraka, ubora na mafanikio.
Alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wenye kasi yenye upendo na hekima na kwamba anamwombea aongoze kwa uadilifu na amani.
Aidha, alimshukuru mkuu wa mkoa Serukamba kwa kuwa kiongozi wa mfano mkoani hapo katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kimaendeleo.
Naye Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Edward Mapunda, alisema maendeleo makubwa aliyoyafanya Rais Samia katika kipindi cha miaka miwili ni ya Watanzania wote, hivyo ni vema wamwombee kwa Mungu aliyetaka wakati huu awe rais wa Taifa hili ili azidi kutekeleza majukumu aliyoitiwa na Mungu.
Awali Serukamba alisema katika kipindi cha miaka miwili ya Utawala wa Mama Rais Samia miradi mingi ya kijamii na kiuchumi imetekelezwa mkoani hapa kutokana na bajeti ya mkoa kuongezwa zaidi ya marudufu.
“Bajeti ya sekretarieti ya mkoa imeongezeka kutoka sh. Milioni 180,187,060,500 mwaka 2020/2021 hadi shilingi 239,808,971,000 mwaka 2022/2023 sawa na asilimia 33.09,” alisema Serukamba.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali Kuu imeidhinisha bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kuwalipa posho madiwani na watendaji kata na posho za mawasiliano watendaji wa vijiji kitendo ambacho hakikuwahi kufanyika katika awamu zote za serikali zilizopita.
