Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Tundu Lissu imeendelea leo, Jumanne Julai 15.2025 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambapo ilikuja kwa ajili ya kutajwa
Katika kesi hiyo ambayo mtuhumiwa Tundu Lissu anajitetea mwenyewe, ilianza kwa Wakili wa Serikali Mkuu Nossor Katuga anayeongoza jopo la Mawakili wa Jamhuri, kuieleza Mahakama kuwa shauri hilo lipo kwenye hatua ya kusomwa na kutolewa maamuzi, na kwamba kwa sasa baada ya upelelezi kukamilika, jalada la shauri husika lilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ambaye amelipitia na kujiridhisha na ushahidi uliopo, na kwamba kwakuwa ameona ushahidi huo umejitosheleza sasa shauri hilo lipo tayari kupelekewa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa
Wakili Katuga, aliendelea kuieleza Mahakama kuwa kufuatia maoni hayo ya DPP, Jamhuri sasa imewasilisha maombi Mahakama Kuu ambayo yanapaswa kusikilizwa kabla ya kupelekwa kwa kesi ya msingi, ambapo amesema maombi hayo ambayo yamepokelewa na kupewa namba 17059 ya mwaka 2025, yamepelekwa kwa kutumia kifungu cha 124 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023
Maombi yaliyowasilishwa na Jamhuri Mahakama Kuu ni yale ya kutaka ‘kuficha’ baadhi ya taarifa zinazopelekea kutambulika kwa mashahidi ikilenga kuwaleta ‘mashahidi (baadhi) wa siri’
Kufuatia kuwasilisha taarifa hiyo Mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Mkuu Nassor Katuga aliiomba Mahakama kuhairisha shauri hilo hadi tarehe nyingine ili kutoa nafasi kwa Mahakama Kuu kusikiliza maombi hayo na kutolea maamuzi, ambapo katika ujenzi wa hoja yake aliieleza Mahakama kuwa Jamhuri imefikia maamuzi ya kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu ili kulinda usalama wa mashahidi wake, na kwamba hairisho la shauri hilo wanaliwasilisha kwa kutumia kifungu cha 265.
