
Kutokana na kifo cha Malkia wa Uingereza Elizabeth wa pili jana Alhamisi jioni, viongozi wa ulimwengu wameendelea kutuma salamu za rambirambi kwa familia yake pamoja na raia wa Uingereza.
Miongoni mwa viongozi waliotoa pole zao ni pamoja na waziri mkuu mpya wa Uingereza, Liz Truss ambaye kupitia taarifa muda mfupi baada ya kifo hicho kutokea, aliandika kwamba “taifa lote limeshtushwa na tukio hilo”, akiongeza kwamba, “Malkia alikuwa msingi imara ambapo Uingereza ya sasa imesimama”.
Rais wa Marekani Joe Biden kwa upande wake amesema Elizabeth alikuwa zaidi ya Malkia aliyetikisa kizazi na pia ameamuru bendera ya Marekani kupeperushwa nusu mlingoti ndani na nje ya nchi kama kumbukumbu yake hadi pale Malkia atakapozikwa.

Mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya ,Ursula von der Leyen, katika ujumbe wake amesema kwamba, “Malkia Elizabeth wa pili alishuhudia vita pamoja na maridhiano, huku akiwa nguzo muhimu katika kuleta mabadilko katika jamii na ulimwengu kwa ujumla”.
