Marekani imeweka vikwazo dhidi ya Rais wa Colombia Gustavo Petro ikidai kwamba ameshindwa kuzuia biashara haramu ya dawa za kulevya nchini mwake, ambapo vizuizi hivyo pia vimemgusa mke wake na mtoto wake mkubwa wa kiume
Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa shirika la habari la kimataifa la Uingereza (BBC) leo, Jumamosi Oktoba 25.2025 imebainisha kuwa kando na familia ya Rais Gustavo Petro, Marekani pia imeweka vikwazo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Colombia Armando Benedetti
Imeelezwa kuwa, miongoni mwa athari zinazowapata wote waliowekewa vikwazo hivyo ni pamoja na kushindwa kuzifikia mali zao zilizopo nchini Marekani
Ikumbukwe kuwa, Colombia hapo awali ilichukuliwa kuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ikipokea mamia ya mamilioni ya dola kila mwaka kutoka Marekani ili kuimarisha vikosi vyake vya kijeshi
Hata hivyo, uhusiano baina ya Rais Gustavo Petro na Rais wa Marekani Donald Trump umekuwa ukisuasua, kwani inadaiwa kuwa Marekani inaiona Colombia kama muuzaji mkubwa wa kokeini Duniani na inasema nchi hiyo inaleta tishio kubwa la dawa za kulevya kwa Marekani, tuhuma ambazo zinakanushwa vikali na Colombia.
