
MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
ILI kunufaika na virutubisho vingi ikiwa ni pamoja na vitamini A na C, madini ya kalisi, potassiam, sodium, chuma, zinki na maganiziam jamii imeshauriwa kutumia Iliki.
Mtaalam wa virutubisho tiba, Abdallah Mandai ametoa rai hiyo leo Machi 23, 2023, jijini Dar es Salaam, katika utaratibu wake wa kutoa nasaha mbalimbali kwa jamii ili kujilinda dhidi ya magonjwa.
“Faida za iliki ni nyingi ambazo ni pamoja na kuipa figo uwezo wa kuondoa taka mwili na kusaidia kuweka sawa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula tumboni. Pia inaondoa hali ya kiungulia na tatizo la kujaa gesi tumboni.
“Kwa wenye tatizo la kukosa choo iliki inasaidia kuondoa tatizo hilo. Saga iliki kisha tumia unga wake kijiko kimoja cha chakula katika uji kwenye kikombe cha chai, fanya hivyo muda wa wiki mbili utapata matokeo bora.
“Kwa mujibu wa utafiti uliowahi kufanywa na Chuo cha Pharmacy of King Saud kilichopo Saud Arabia, ulibaini iliki ina uwezo mkubwa wa kuboresha mishipa ya damu kwenye moyo na hivyo kuulinda dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mfumo wa moyo,” amesema Mtaalam huyo.
Pia Mtaalam Mandai amebainisha kuwa vilevile iliki inasaidia kuondoa tatizo la maradhi ya kinywa kinachotoa harufu mbaya na kutibu vidonda vya mdomoni na matatizo ya kinywa kwa ujumla.
“Tumia unga wa iliki uliochanganywa na maji ya uvuguvugu kwa kusukutua mdomoni kila siku muda wa wiki tatu. Pia iliki inasaidia wenye matatizo ya maambukizi kwenye njia ya mkojo sanjari na kupambana na magonjwa mbalimbali yakiwamo yanayoambukiza kwa njia ya kujamiiana.
“Kwa mujibu wa Kitengo cha Kilimo na Lishe nchini Marekani, iliki ina carbohydrates gramu 68, protini 11 na nyuzinyuzi gramu 2.
“Kijiko kimoja cha chakula cha unga wa iliki tumia katika kikombe cha chai chenye uji mwepesi. Fanya hivyo muda wa wiki mbili utapata nafuu na hata kupona kabisa hapa ni kwa magonjwa ya kujamiiana.
“Iliki pia inasaidia kukabilina na hali ya maambukizi ya mafua na kikohozi pamoja na kuondoa maumivu ya viungo vya mwili. Dalili za matatizo ya saratani ya shinikizo la damu iliki inaweza kuwa suluhisho inapotumika kwa maelekezo ya mtaalamu.
“Kiungo hiki adhimu kina uwezo wa kuondoa dalili za tatizo la pumu na matatizo kwenye mfumo wa hewa. Pamoja na hayo kiungo hiki pia ni mujarabu kwa kufifisha hali ya kichefuchefu na hivyo kumsaidia mgonjwa mwenye hali hiyo kutotapika.
“Iliki inapochanganywa na unga wa mdalasini inasaidia kupunguza maumivu ya koo,” ametanabahisha Mtaalam Mandai.
Mtaalam Mandai anayetoa huduma za kiafya kwa kutumia virutubisho tiba asili anamkaribisha yeyote mwenye tatizo la kiafya katika kituo chake cha kutolea huduma za afya, Ukonga Mongo la Ndege, jijini Dar es Salaam.
