Mamia ya watu wanahofiwa kufariki dunia katika mji wa Mayotte baada ya eneo la Bahari ya Hindi ya Ufaransa kuathirika na kimbunga kikali.
Makazi yote yaliharibiwa wakati Kimbunga Chido kilipotua kwa kasi ya upepo wa zaidi ya 225km/h (140mph) na kusababisha watu kuishi katika makazi ya muda hasa walioathirika zaidi.
Wafanyakazi wa uokoaji wanatafuta manusura katika maeneo yenye vifusi.
Uharibifu mkubwa wa miundombinu na nyaya za umeme zilizoanguka na barabara zisizopitika unazuia kuendelea kwa shughuli za dharura.
Mkazi mmoja wa jiji kuu, Mamoudzou, akiwa anasubiri kwenye foleni ili apate msaada wa mahitaji muhimu alisema: “Hatujapata maji kwa siku tatu, na sasa hali imeanza kuwa ngumu. Tunajitahidi kupata hata kidogo tu ili tuweze kuishi, kwa sababu hatujui maji yatarudi lini.”
Mkazi mwingine wa Mamoudzou, John Balloz, alisema bado anashangaa jinsi alivyokwepa mauti wakati kimbunga hicho kilipopiga.
“Ilikuwa ni upepo, upepo ulivuma, na niliogopa, nilipiga kelele, ‘Tunaomba msaada.’ Nilikuwa ninapiga kelele kwa sababu niliona mwisho wa maisha yangu ukiwadia,” alisema.
Jamii maskini za Mayotte, ikiwa ni pamoja na wahamiaji wasio na vibali ambao wameingia katika eneo la Ufaransa katika jitihada za kuomba hifadhi, wanafikiriwa kuwa ndio waathirika zaidi kutokana na mazingira magumu ya makazi yao.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa pole zake kwa “watu wa nchi yetu huko Mayotte, ambao wamepitia magumu ndani ya saa chache za kutisha zaidi, na wengine, wamepoteza kila kitu, maisha yao”
Chanzo: BBC
