
Waziri wa Nishati, January Makamba amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye Mkutano wa Viongozi wa Dunia unaojadili Program ya Afrika ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, unaofanyika nchini Uholanzi.
Mkutano huo uliofanyika jana Jumatatu Septemba 5, 2022 unalenga kushawishi washirika wa maendeleo, taasisi za kifedha, sekta binafsi na marafiki wa Afrika kuchangia fedha kwenye Programu hiyo ya Afrika ambayo inahitaji Dola za Marekani Bilioni 25 ifikapo 2025.
Benki ya Maendeleo ya Afrika imechangia Dola za Marekani bilioni 12.5.
Mkutano huu unafanyika kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya Tabia Nchi ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu, Sharm El Sheik Misri ambako suala la kuhimili mabadiko ya Tabianchi kwa Afrika ni moja ya agenda muhimu.
Katika Mkutano huo Waziri wa Nishati amekutana na Viongozi wa Dunia, Wakuu wa Taasisi na Mashirika mbalimbali na kujadiliana nao fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna bora ya Tanzania kunufaika na Mpango huo wa AFRICA ADAPTATION ACCELERATION PROGRAM (AAAP) ambao utaharakisha mipango ya nchi katika kukabiliana na majanga yakiwamo UVIKO19, ukame, njaa, ajira kwa vijana na mafuriko.
Mkutano huo uliongozwa na Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Macky Sally, na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa pia Mwenyekiti wa Kituo cha kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (GCA), Ban Ki-Moon.
