
Mchakato wa uokoaji unaendelea Mashariki mwa Afghanistan baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea nchini humo na kuua watu wapatao 1,000 huku wengine maelfu wakiachwa bila makazi.
Mkuu wa idara ya mawasiliano katika mkoa wa Paktika, Mohammad Amin Huzaifa, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, kuna changamoto ya kupata taarifa zaidi kutoka eneo la tukio kutokana na hitilafu ya mitandao.
Huzaifa ameeleza kuwa hakuna taarifa zaidi kuhusu idadi ya waliofariki. Amesema waokoaji wanakumbwa na changamoto kwa sababu eneo la tukio limeathirika na mafuriko baada ya mvua kubwa iliyonyesha jana usiku.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema shirika hilo litapeleka madaktari, chakula, na vifaa vyingine kuwasaidia wahanga wa tetemeko hilo la ardhi.
