Mamlaka za Marekani zimewashtaki Rais wa zamani wa Venezuela, Nicolás Maduro, pamoja na mkewe Cilia Flores, kwa madai ya kula njama ya kuwatesa raia wa Venezuela ili kulinda utawala wake madarakani. Mashtaka yaliyorekebishwa yanamtuhumu Maduro kuidhinisha matumizi ya mateso dhidi ya watu maalum na kusimamia mfumo uliotumia mateso, kuwekwa kizuizini kiholela na vurugu kuwanyamazisha wapinzani wa kisiasa.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, maelfu ya raia wa Venezuela walidaiwa “kunyanyaswa, kutishiwa, kukamatwa, kushtakiwa, kushambuliwa, kuteswa au kuuawa” na watu waliokuwa wakitenda kwa niaba ya Serikali ya Maduro. Miongoni mwa tuhuma zilizotajwa ni matumizi ya mshtuko wa umeme, vipigo na kuwanyima waathirika hewa.
Hati hiyo pia inamtuhumu Maduro kuidhinisha mbinu mbalimbali za mateso na, katika tukio moja, kumtishia mfungwa kumuua mtoto wake kama njia ya kumtesa kisaikolojia. Toleo jipya la hati hiyo limetaja pia madai ya kuhusika kwa taasisi ya ujasusi wa kijeshi ya Venezuela, DGCIM, ambayo imekuwa ikihusishwa na ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa.
Mashtaka hayo yanaongeza shinikizo la kisheria dhidi ya Maduro, ambaye tayari anakabiliwa na tuhuma nchini Marekani za kula njama ya kusafirisha kwa magendo cocaine kwenda nchini humo. Maduro na Flores wamekuwa wakishikiliwa New York tangu Januari, baada ya majeshi ya Marekani kuwakamata katika operesheni ya usiku nyumbani kwao Caracas.
Maduro na Flores wamekanusha mashtaka ya usafirishaji wa dawa za kulevya na wamejibu mahakamani kuwa hawana hatia. Iwapo watapatikana na hatia katika mashtaka hayo, wanaweza kukabiliwa na kifungo cha maisha jela.
Maduro pia amekuwa akichunguzwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutokana na madai ya uhalifu dhidi ya ubinadamu unaohusishwa na ukandamizaji dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa. Hata hivyo, Maduro amekuwa akikanusha mara kwa mara tuhuma za kufanya makosa.
