Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA), Majula Kapumu, amewaomba radhi abiria kwa usumbufu uliotokana na kusitishwa kwa baadhi ya safari, huku akisema malalamiko ya madereva yamepokelewa na Serikali na yanaendelea kushughulikiwa.
Kapumu amesema wanatambua kuwa abiria ndio wanaobeba athari kubwa pale huduma za usafiri zinapokwama, hivyo ametoa pole na kuomba msamaha kwa usumbufu uliojitokeza. Amesema Serikali imepokea changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili madereva, huku viongozi wao wakikutana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na viongozi wengine wa Serikali kwa ajili ya kuzifikisha hoja hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kutetea Taaluma ya Madereva Tanzania, Yohana Mwanyaga, amewataka madereva na wadau wa usafirishaji kutumia mazungumzo kutatua changamoto zinazojitokeza badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuwaathiri wananchi.
