
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limewatia mbaroni watu watatu, baada ya kuwakamata na vipande 25 vya meno ya tembo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, amesema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya oparesheni maalum ya kuzuia uhalifu iliyofanyika kuanzia Februari 25, hadi Machi 9,2022.
Amebainisha kuwa katika opareheni hiyo jeshi hilo kwa kushirikiana na Kikosi Kazi cha Kuzuia na kupambana Ujangili eneo la Ubungo NHC, Dar es Salaam, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na vipande 25 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 20.9.
Asema katika uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi hilo umebaini meno hayo ni sawa na Tembo 14 walio uawa yalikutwa yakiwa yamefichwa katika moja ya nyumba ya watuhumiwa hao ambapo pia lilikutwa gari lenye namba ya usajili T. 818 DCA Toyota Wiills iliyotumika kuyasafirisha.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Gabriel Mgana, mkazi wa Ubungo NHC 2, Haffarman Yona maarufu kama Mnyaturu na Felician Cyril (57), wote wakazi wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
“Jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kujua Tembo waliouawa ni wa eneo lipi na thamani ya meno hayo ni kiasi gani na yalikuwa yanatarajiwa kupelekwa au kuuzwa wapi,” amesema Kamanda Muliro.
