
Serikali mkoani Pwani imeziagiza halmashauri zote mkoani humo, kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaposhukiwa kufanya mambo kinyume na kiapo cha ajira zao.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa huo, Aboubakar Kunenge, wakati wa mkutano wa baraza la madiwani lilipojadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG ), kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Kunenge amesema ni wakati wa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi ambao watabainika kujinufaisha kwa mapato ama kusababisha hasara kwa halmashauri husika.
Aidha, ameiagiza halmashauri ya mji wa Kibaha na halmashauri ya Wilaya Kibaha kuhakikisha zinafunga hoja zote ambazo hazijafungwa katika ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/2020, kabla ya Septemba 30 mwaka huu.
Mkuu huyo wa mkoa wa Pwani ameongeza kuwa adhabu itakayotolewa dhidi ya mshukiwa ilingane na ukubwa wa tuhuma husika aliyosababisha ili kusaidia kulinda maadili na uwajibikaji.
Pamoja na hayo amewaasa watumishi kuacha kuridhika na vyanzo vya mapato walivyovizoea badala yake wabuni vipya pamoja na miradi ya kimkakati itakayowawezesha kuinua mapato yao ya ndani.
Naye mkaguzi mkuu wa hesabu mkoani Pwani, Mary Dibogo, amesema wao wapo kwa ajili ya kufanya ukaguzi kwa maslahi ya jamii na serikali, hivyo CAG hawezi kuionea halmashauri yoyote.
