
Mkurugenzi wa halmashauri Ikungi Justice kijazi
DOTTO MWAIBALE, IKUNGI
MKURUGENZI mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi, amesema moja ya mafanikio makubwa waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (Veta).
Kijazi aliyasema hayo juzi wakati wa kupokea taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili tangu Rais Samia aingie madarakani na kumpongeza kwa mambo makubwa ya maendeleo yaliyofanyika katika kipindi hicho katika wilaya ya Ikungi na mkoa wa Singida kwa ujumla.
Alisema ujenzi wa chuo hicho ni fahari kwao kwani kitaanza kutoa mafunzo ya ufundi wa aina mbalimbali kwa vijana wa wilaya hiyo na wilaya jirani jambo ambalo litawasaidia vijana hao kujiajiri na kuajiriwa katika maeneo tofauti kulingana na fani zao za ufundi watakazokuwa wamejifunza.
“Tulikuwa na changamoto kubwa ya vijana wetu wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari kwenda kupata elimu ya ufundi nje ya wilaya yetu lakini kukamilika kwa ujenzi wa chuo cha Veta hapa Ikungi kunakwenda kuondoa changamoto hiyo, nampongeza sana Rais wetu Dk. Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki,” alisema Kijazi.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Veta Kanda ya Kati, John Mwanja, akizungumzia ujenzi wa chuo hicho alisema kina umiliki wa Hati namba: 2218- SGD na kimejengwa katika kijiji cha Muungano, kata ya Unyahati, kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 50.
Alisema mradi huo wa ujenzi ulioanza mwezi Machi, 2020, ukisimamiwa na chuo cha Veta Singida ambapo ulipaswa kutekelezwa kwa muda wa miezi sita, lakini haukukamilika kwa wakati hadi mwaka huu.
Alifafanua kuwa mkurugenzi mkuu wa Veta Singida, Februari 28, mwaka jana (2022) alihamishia majukumu ya usimamizi wa ujenzi huo kutoka Chuo cha Veta Singida kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Veta Kanda ya kati ambaye hadi sasa kinaendelea kujengwa kwa mfumo wa “Force Account”.
Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi huo alisema unahusisha majengo 17 ambayo ni pamoja na jengo la utawala, majengo manne ya karakana, jengo la madarasa mawili makubwa, majengo mawili ya mabweni (wasichana na wavulana), bwalo la chakula na jiko pamoja na majengo matatu ya vyoo (wasichana wavulana na watumishi).
Mengine ni nyumba mbili za watumishi, jengo la umeme, jengo la bohari na kibanda cha mlinzi ujenzi ambao umefikia wastani wa asilimia 96.
Alifafanua kuwa Chuo hicho kitakapokamilika, kitaendesha mafunzo ya kozi ndefu na fupi na kwamba kozi za muda mrefu zitachukua muda wa miaka miwili hadi mitatu ambazo zitatolewa katika fani sita katika awamu ya kwanza mara chuo kitakapokamilika ambazo ni uhazili na kompyuta, ushonaji, uashi, ufundi umeme wa majumbani, ufundi magari na uchomeleaji vyuma.
Alisema chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 240 wa kozi ndefu na 144 wa bweni ambapo wasichana 64 na wavulana 80.
Alibainisha pia kutakuwa na mafunzo ya muda mfupi yatakayochukua mwezi mmoja hadi miezi sita kwa wastani mafunzo hayo yanakadiriwa kudahili wanafunzi 250 hadi 900 kwa mwaka kulingana na mahitaji ya jamii na shughuli za kiuchumi za eneo hilo.
Mwanja alisema hadi sasa sh. bilioni 2.3 zimeshatumika katika ujenzi huo ambao utatarajia kukamilika mwezi ujao wa Aprili ambapo Serikali imetoa sh. milioni 259 ili kukamilisha ujenzi huo. Alisema chuo hicho kitakapokamilika kinatarajiwa kuhudumia wakazi 343,985 wa wilaya ya Ikungi na wengine 1,754,370 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Singida.
