
Kikao cha bunge kilichopangwa kufanyika leo Jumanne kujadili ripoti iliyogundua kuwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa huenda alikiuka katiba kimeahirishwa kwa wiki moja.
Ripoti hiyo imesema Ramaphosa anadaiwa kuficha wizi katika shamba lake. Amekana kufanya makosa yoyote huku msemaji wake akisema ripoti hiyo ‘ina dosari’.
Kamati ya upangaji ya Bunge ilikutana jana Jumatatu usiku na kukubaliana kwa kauli moja kufanya mjadala huo Desemba 13 ili kuruhusu wabunge kusafiri hadi Cape Town ambako bunge linakaa.
Mjadala kuhusu ripoti hiyo unaweza kuamua iwapo atamshtaki Rais Ramaphosa, ingawa chama tawala cha ANC kimetangaza kuwa kitapiga kura kupinga jaribio hilo.
Rais alikwenda mahakamani jana Jumatatu kuomba amri ya kutangaza hatua zozote zilizochukuliwa na bunge kufuatia kutolewa kwa ripoti hiyo kuwa batili na kinyume cha sheria.
Iwapo itakubaliwa, agizo hilo lingetumika kwa kura ya wabunge ambayo itatoa nafasi ya kuanzishwa upya mchakato wa kumuondoa madarakani.
