
Kiongozi wa mwisho wa uliokuwa Umoja wa Kisovieti, Mikhail Gorbachev, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91.
Kulingana na taarifa ya hospitali ya mjini Moscow, Gorbachev amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini taarifa hiyo haikueleza zaidi.
Viongozi mbali mbali wa kimataifa wametuma salamu zao za rambirambi baada ya kifo hicho, wakimsifu Gorbachev kama mpenda amani aliyehitimisha enzi ya Vita Baridi.
Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, amesema Rais Vladimir Putin amesikitishwa na kifo cha Gorbachev.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amemuelezea Gorbachev kama kiongozi aliyebadilisha mkondo wa historia ya dunia, huku rais wa Marekani Joe Biden akisema Mikhail Gobachev alikuwa na maono yaliyomwezesha kuona mustakabali tofauti wa dunia, na akaitoa muhanga kazi yake kuyatimiza.
Shirika la habari la Urusi, TASS, limesema kiongozi huyo atazikwa katika makaburi ya heshima kubwa ya Novodevichy mjini Moscow.
