
Mahakama ya kijeshi ya mjini Ougadougou (Wagadugu), nchini BurkinaFaso, imeanza kusikiliza kesi iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu dhidi ya watu 14 akiwamo rais wa zamani wa nchi hiyo, Blaise Compaore.
Compaore na wenzake wanatuhumiwa kwa mauaji ya kiongozi mwanamapinduzi, Thomas Sankara, miaka 34 iliyopita.
Sankara mwanamajumui maarufu barani Afrika, aliuawa pamoja na watu wengine 12 kwa kupigwa risasi na kundi la wauaji Oktoba 15 mwaka 1987 wakati wa mapinduzi yaliyomuingiza madarakani rafiki yake na mshirika wake kwenye mapambano Blaise Compaore.
Wiki iliyopita Compaore alitangaza kupitia mawakili wake kwamba atasusia kesi hiyo.
Yeye pamoja na mshirika wake wa karibu jenerali Gilbert Diendere aliyewahi kuongoza kitengo maalum cha usalama wa rais wanakabiliwa na tuhuma za kuhusika na mauaji, kuvuruga usalama wa taifa na kuhusika na njama za kuificha miili ya waliouawa.
Hyacinthe Kafando, ambaye ni ofisa mwingine maarufu katika kesi hiyo, aliwahi kuwa mkuu wa majeshi katika kikosi cha ulinzi wa rais Compaore anayetuhumiwa kuongoza kundi la watu waliokuwa na silaha naye yuko mafichoni anatafutwa. Blaise Compaore siku zote amekuwa akisema kesi hiyo ni ya kisiasa.
