Upande wa Jamhuri umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuzuia urushaji wa moja kwa moja (Live) wa mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kwa lengo la kulinda utambulisho wa mashahidi.
Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ametoa ombi hilo leo Jumatano Julai 13, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, akibainisha kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania tayari ilishatoa maagizo ya kuhakikisha mashahidi ambao ni raia wanalindwa dhidi ya utambulisho usioidhinishwa.
Kwa mujibu wa Wakili Katuga, maagizo ya Mahakama Kuu yalipiga marufuku uchapishaji au uwasilishwaji wa ushahidi wowote unaoweza kufichua utambulisho wa mashahidi raia wa kawaida bila ruhusa maalum ya mahakama hiyo.
“Ombi letu, pamoja na nia njema ya mahakama kuonesha mwenendo wa shauri kwenye vyombo vya habari, ni kwamba yafuatwe maagizo ya Mahakama Kuu. Ikiwa mshtakiwa atasomewa mashtaka, basi iwe kwenye mahakama ya wazi lakini bila matangazo ya moja kwa moja (Kwenye tv au radio),” amesema Katuga.
Kwa upande wa Lissu amesema anapinga maombi ya upande wa Jamhuri wa kufuta kuonyeshwa kwa kesi hiyo na vyombo vya Habari kwa sababu anaogopa kesi kufanyika gizani yaani Star Chamber. Alidai kufanya hivyo kuna hatari ya kumnyima haki mshitakiwa.
Hakimu Kiswaga alisema ataahirisha shauri kwa ajili ya kufanya maamuzi na atatolea amri na kuendelea na comital. Lissu alimuomba hakimu kupanga siku za karibuni na Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18 mwaka huu.
