
Gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda limeripoti kuwa wafanyabiashara nchini humo wanaouza kuku na mayai nchini Kenya hutozwa shilingi 70 za Kenya sawa na sh. 2500 ili kupata idhini ya kuingiza mayai yao Kenya.
Wafanyabiashara hao pamoja na vyama vyao wameliambia gazeti hilo kuwa jambo hilo linalokwenda kinyume na makubaliano ya awali na kwamba tozo hizo ni miongoni mwa masharti ambayo yamewekwa dhidi ya mayai kutoka Uganda.
Hii inakuja miezi sita baada ya Kenya kuondoa marufuku iliyokuwa imeiweka dhidi ya kuku na bidhaa zake kutoka Uganda kwa ajili ya kuwalinda wakulima wake na athari za Covid-19.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa mwezi Januari na Waziri wa kilimo wa Kenya Peter Munya, Waziri wa biashara Betty Maina, na Waziri wa kilimo wa Uganda, Frank Tumwebaze ilionesha kuwa Kenya itaruhusu mauzo ya mayai, kuku na vifaranga, baada ya kuzuiwa kuingia nchini Kenya tangu Februari 2021.
