
Kamati ya Tathmini ya Mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST), imesema imewasilisha majina ya wakufunzi waliotajwa kwa Uongozi wa juu wa Taasisi ili uweze kufuatilia mienendo yao.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwapo tuhuma za vitendo vya rushwa, uonevu, upendeleo katika utungaji au usahihishaji wa Mitihani ya Wakufunzi hao na kupelekea kufeli kwa idadi kubwa ya Wanafunzi wa Taasisi hiyo Kundi la 33 la mwaka wa masomo 2021-2022.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, Mwenyekiti wa Kamati, Dk. Harrison Mwakyembe amesema endapo tuhuma hizo zitaendelea Wakufunzi hao wahamishiwe idara nyingine za Serikali ili kulinda taswira ya Taasisi.
Kupitia taarifa hiyo, Dk. Mwakyembe amesema Kamati inaona kuwa ni wajibu wa Taasisi kuweka mazingira rafiki kwa Wanafunzi katika Taasisi hiyo sanjari na ukarabati wa Miundombinu ya Taasisi ili kuwa na mazingira bora kwa Wanafunzi hao kujisomea na kufaulu masomo yao vizuri.
Aidha, Kamati hiyo imebaini kuwa Taasisi hiyo ya ‘Law School of Tanzania’ hakuna Mahakama ya kufundishia kwa vitendo kwa Wanafunzi wanaosoma hapo huku ikifafanua kuwa mahakama iliyojengwa katika Taasisi hiyo bado inatumiwa na Mahakama Kuu ya Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na kushindwa kutoa mchango kwa Wanafunzi wa Taaluma ya Sheria wanaofanya mafunzo yao kwa vitendo.
“Kamati inatoa rai kwa Wizara na Mahakama ya Tanzania kuitafutia Divisheni hiyo ya Mahakama Kuu mapema iwezekanavyo sehemu nyingine ili kuruhusu kwa ushirikiano na Mahakama ya Tanzania kuanzishwa kwa Mahakama ya Wilaya itakayotumika kikamilifu katika kuimarisha mafunzo ya uanasheria kwa vitendo LST”, imeeleza Kamati
Kamati hiyo yenye Wajumbe Sita waliokuwa chini ya Mwenyekiti, Dk. Mwakyembe imewasilisha taarifa hiyo kwa Waziri Dk. Ndumbaro baada ya kuwapo mjadala mkubwa nchini baada ya kutangazwa matokeo ya Mitihani ya ‘Law School ya Kundi la 33 la mwaka 2021-2022, mapema mwezi Oktoba.
Katika matokeo hayo, Wanafunzi 633 wa Kundi hilo walifanya Mitihani hiyo, Wanafunzi 26 walifaulu Mitihani katika mkao wa kwanza, Wanafunzi 342 walifaulu baadhi ya masomo na wana fursa kurudia Mitihani ya masomo waliyoshindwa, wanafunzi 265 walifeli Mtihani mzima na wanaweza kuanza upya mafuzo wakiwa tayari.
