
Corneille Nangaa, aliyewahi kuwa mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amehamasisha mapinduzi makubwa nchini humo. Kutoka kusimamia uchaguzi wenye utata wa mwaka 2018 hadi kuwa mshirika mkubwa wa M23, kundi lenye uasi mkubwa dhidi ya Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, safari yake imekuwa ya kushangaza sana.
Sasa akiwa mkuu wa chama cha CRA (Congo River Alliance) na mshirika mkubwa wa M23, kundi la waasi linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda,Linaloongozwa na kamanda Mkuu Sulatani Makenga, Nangaa amechukua udhibiti wa miji muhimu, ikiwa ni pamoja na Goma, na ametangaza kuunda ungozi mpya mjini Goma nia ya kuendelea hadi Kinshasa.
Akiwa amehukumiwa kifo kwa mashitaka ya uhaini na uhalifu wa kivita, Nangaa anasalia kuwa mhusika mkuu katika mzozo unaozidi kupamba moto nchini DRC. Je, Nangaa aliwezaje kufikia hatua hii?
Historia na Safari Yake ya Kisiasa Nangaa alizaliwa tarehe 9 Julai 1970 katika jimbo la Haut-Uele. Alianza maisha yake mbali na uwanja wa vita, akihitimu shahada ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Kinshasa kabla ya kufanya kazi na mashirika ya kimataifa, yakiwemo Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP).
Mafanikio yake ya kisiasa yalikuja mwaka 2015 alipochaguliwa kuwa Rais wa Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) chini ya utawala wa Rais wa wakati huo, Joseph Kabila.
