
Mamlaka nchini Rwanda zimesema Rais wa Nchi hiyo, Paul Kagame, amemsimamisha kazi waziri wake wa vijana na utamaduni, Edouard Bamporiki.
Taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu imesema kusimamishwa kwa Bamporiki kumetokana na “masuala ya uwajibikaji yaliyo chini ya uchunguzi”.
Wachunguzi wa serikali wamesema amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani wakati uchunguzi ukiendelea. Bamporiki, 39, awali alikuwa mfuasi mkuu wa Rais Kagame na chama tawala.
Ana uwepo mkubwa kwenye mitandao ya kijamii na anachukuliwa kuwa mwanasiasa mwenye utata katika baadhi ya maeneo.
Akiwa mshairi, mtayarishaji wa filamu na mwigizaji maarufu wa tamthilia ya redio alikuwa kwenye baraza la mawaziri tangu 2019 na hapo awali alikuwa mbunge.
Bado hajazungumza lolote kuhusu tuhuma za ufisadi zinazomkabili.
