Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro, amewataka askari Polisi kutumia weledi na nidhamu wanapotoa huduma kwa jamii.
IGP Sirro ametoa kauli hiyo jana wakati wa sherehe za mahafali ya Sita ya Vyuo vya Taaluma vya Polisi yaliyofanyika Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Amesema mafunzo yanayotolewa na vyuo ya Polisi yanalenga kuinua kiwango cha ujuzi na kuwaongezea maarifa askari Polisi katika kuboresha utendaji kazi za Jeshi hilo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Vyuo vya Polisi, Profesa Frolence Luoga, amewataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kulisaidia Jeshi hilo kuhakikisha suala la usalama wa raia na mali zao linazidi kuimarika.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro, Kamishna msaidizi Mwandamizi (SACP), Ramadhani Mungi, wakati akitoa tathmini ya uendeshaji wa vyuo ya Polisi, amesema jumla ya wahitimu 305 waliohitimu jana watatumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kutoa huduma bora na zenye viwango kwa Jeshi hilo na raia.

