
Mtaalam wa virutubisho tiba, Abdallah Mandai, amesema mbarika au nyonyo ni miongoni mwa mimea tiba yenye ufanisi mkubwa katika kutibu maradhi mengi.
Amesema mmea huo maarufu ni tiba ya kifua kikuu ambapo mizizi na kikonyo ni tiba anuai ya magonjwa ya kwikwi.
Mtaalam huyo ametoa kauli hiyo leo Aprili 4, 2022, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumzia aina mbalimbali ya mimea tiba inavyosaidia kutibu magonjwa mbalimbali.

“Matatizo ya mafindofindo, kuugua macho, maumivu ya mgongo, ugonjwa wa manjano, uvimbe kooni, maumivu ya miguu, kisonono, kaswende, kuondoa kondo la nyuma na tatizo la kwikwi mbarika ni msaada mkubwa,” amesema.
“Kwa maradhi ya kaswende, ponda mizizi ya mbarika, chemsha, kunywa glasi moja ya maji hayo mara mbili kutwa muda wa siku saba.
“Kama una tatizo la kwikwi jaza maji kwenye kikonyo, mpe mgonjwa anywe kila baada ya dakika 3 hadi kwikwi iishe.
“Kwa maumivu ya mgongo, pasha majani ya nyonyo kanda mgongo unaouma asubuhi na jioni utaondokana na tatizo lako.
“Ikiwa unaumwa miguu, pasha katika moto majani ya nyonyo kisha funga katika mguu wenye maumivu, badilisha majani kila baada ya muda fulani.
“Kama mzazi ana tatizo la kutoka kondo la nyuma atafune mizizi ya mbarika kabla ya uchungu itamsaidia mfuko wa uzazi kutoka kwa urahisi na usalama zaidi wakati wa kujifungua.
“Ikiwa umeungua moto menya mbegu za mbarika meza kwa glasi moja ya maji kila siku muda wa siku tano zinasaidia kuondoa maumivu na kuponya kidonda.
“Mafuta yanayotokana na mbegu za nyonyo yanasaidia kuondoa tatizo la jongo au gauti linalowakumba hususan wale wanaoishi maeneo ya baridi kali.
“Mafuta ya mbarika pia yanaweza kutumika kama njia ya
kupanga uzazi kwani yana kiasi fulani cha sumu ijulikanayo kitaalamu kama ricin ambayo ikitumiwa kwa kiasi kidogo ina uwezo wa kukosesha kutungwa mimba. Hata hivyo namna ya kutumia unatakiwa umwone mtaalamu.
“Mafuta ya ricinoleic yanayotokana na nyonyo yanasaidia kurekebisha mzunguko wa hedhi kwa mwanamke hususan kwa yule inayowahi au kuchelewa.
“Mafuta ya nyonyo pia ni kiboko kwa magonjwa mbalimbali ya ngozi yanayosababishwa na bakteria.
“Mnyonyo unaweza pia kuwafaa watu wanaoishi na Virus Vya Ukimwi (VVU) kwani mafuta yake ni sumu ya kuua vimelea vya magonjwa kama vile bakteria na ukungu.
