
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imeongeza idadi ya wanyamapori katika hifadhi ndogo ya asili ya Luhira iliyopo katikati ya mji wa Songea, mkoani Ruvuma.
Akizungumza baada ya kuwafikisha wanyama hao kwenye hifadhi ya Luhira, Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori wa TAWA, Asharaf Shemoka, amesema wanyamapori walioletwa katika hifadhi hiyo ni nyumbu watatu kati yao dume mmoja na pofu watatu kati yao majike wawili.
Amesema wanyamapori hao wametolewa katika Shamba la ufugaji la wanyamapori Majichai, iliyopo halmashauri ya wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha na kwamba wanyama hao licha ya kusafiri umbali mrefu wamefika Songea wakiwa na hali nzuri.
Hata hivyo,amesema huo ni mpango wa awali wa kuleta wanyamapori katika hifadhi ya Luhira na kwamba wanatarajia kuongeza wanyama zaidi wakiwamo mbuzi mawe, kongoni, swalapala na wanyama wengine kadiri itakavyowezekana.
Kwa upande wake, mkuu wa kikosi dhidi ya ujangili kanda ya Kusini (KDU), ambaye pia ndiye Msimamizi Mkuu wa Hifadhi ya Luhira, Keneth Sanga, amesema baada ya kuongeza idadi ya wanyamapori sasa wanatarajia pia idadi ya watalii itaongezeka.
