
Spika wa Bunge Dk.Tulia Ackson ameliambia bunge jijini Dodoma kuwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki ni mahakama, hivyo, kwa sasa hawezi kusema chochote kuhusu hatma ya viti 19 vya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliofukuzwa uanachama vipo wazi, kwa kuwa suala hilo lipo mahakamani.
Dk. Tulia amesema kwa kuwa tayari alipokea barua kutoka kwa wabunge hao 19 wakimtaarifu kuwa tayari wamefungua shauri mahakamani kupinga kufukuzwa uanachama, Bunge haliwezi kuingilia mchakato wa mahakama na badala yake linalazimika kusubiri hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi wake.
Spika amesema alipokea barua za wabunge hao zikieleza kuwa uamuzi uliotolewa na Chadema dhidi yao si halali, ni kinyume, haukuzingatia haki ya msingi ya kuwasikiliza, kujitetea.
Wabunge hao wamefungua rufaa mahakamani ya kupinga uamuzi huo.
Ofisa wa Chadema alitumwa kupeleka barua kwa Spika wa Bunge na kisha kuambiwa asubiri lakini alipokea simu kutoka kwa viongozi wa Chadema wakimtaka aondoke eneo hilo na hivyo watafanya utaratibu mwingine wa kuituma barua hiyo.
“Ninalazimika kutotangaza kwamba nafasi 19 za wabunge wa Viti Maalum Chadema hazitabaki wazi hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi.
“Kama kutakuwa na swali lolote msemaji wa mwisho wa jambo hili ni Spika wa Bunge na si yeyote,” amesema Dk. Tulia.
Mei 12, 2022, Baraza Kuu la Chadema lilitupilia mbali rufaa ya wabunge hao ambao walikuwa wakipinga kufukuzwa uanachama na Kamati Kuu ya chama hicho, na hivyo kumlazimu Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika, kuwasilisha barua kwa Spika kumtaarifu kuhusu jambo hilo ili aendelee na taratibu nyingine.
