
Mtoto Gindu Kululu (06), mkazi wa mtaa wa Iyoma, kata ya Somanda, halmashauri ya mji wa Bariadi, mkoani Simiyu, ameshambuliwa na fisi usoni.
Matukio ya mnyama fisi kushambulia watoto na kuwajeruhi maeneo ya usoni na kichwani yamezidi kushamili katika mji wa Bariadi.
Wazazi wa mtoto huyo wamesema tukio hilo limetokea jana Mei 2, saa 2 asubuhi nyumbani kwao ambapo mtoto huyo alikuwa nje ya nyumba yao ghafla alivamiwa na mnyama huyo ambaye alitokea vichaka vilivyopo karibu na nyumba hiyo.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya mji wa Bariadi Emmanuel Costantine amethibitisha kupokelewa mtoto huyo na kwamba hali yake inaendelea vizuri.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange akiwa na kikosi cha askari wa kutuliza ghasia (FFU), walimsaka fisi huyo na kufanikiwa kumuua.
