
Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki (EALA,) linakusudia kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi pekee mwanamke Afrika Mashariki na anayeonesha mwelekeo mzuri katika kusimamia demokrasia.
Wakizungumza mwishoni mwa wiki katika Bunge la Nne linalofanyika makao makuu ya jumuia hiyo, jijini Arusha, wabunge kutoka Tanzania Dakta Abdulah Makame, Adam Kimbisa na Mariam Ussi wamesema bunge hilo limejipanga kutoa mwaliko maalumu kwa Rais Samia ili aende katika bunge hilo nao wampe pongezi zake.
Kimbisa ambaye pia ni Mwenyekiti wa wabunge wa EALA kutoka Tanzania, amesema kiu ya wabunge wa bunge hilo ni kuona Rais huyo akisimamia vema demokrasia katika uongozi wake.
Kwa upande wake mbunge Ussi Yahaya amesema Bunge hilo la Afrika Mashariki limeamua kumpongeza kwa dhati Rais Samia na lipo tayari kufanya naye kazi ya kuijenga jumuia hiyo.
Ameongeza kuwa pamoja na hatua hiyo ya Bunge la EALA wao kama wabunge wa wanawake kutoka Tanzania wanakusudia kumwalika ili kumpongeza.
Naye Dakta Abdulah Makame amesema Bunge hilo limeunga mkono hoja iliyotolewa ya kumpongeza Rais Samia na kuadhimia aalikwe na kulihutubia ili kutoa mawazo yake kuhusu masuala ya mtangamano wa jumuia hiyo.
Katika hatua nyingine, Dakta Makame amewasilisha hoja binafsi ya kutaka bunge hilo liwe na bendera yake inayojitegemea ili kuweza kushushwa nusu mringoti pindi kutatokea majanga mbalimbali ikiwamo mbunge kufariki kama sehemu ya kutoa heshima ya kumuenzi marehemu.
