Chama Cha.Mapinduzi (CCM) kimewaonya Wanasiasa kutoingilia masuala ya ardhi na malipo katika maeneo ya Bumbwini na Mangapwani mkoa wa kaskazini Unguja kwa lengo la kuichafua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Aidha CCM kimesisitiza kusimamia kwa nguvu zote na kuhakikisha malipo yote ya wananchi yanalipwa na hakuna mtu atakaedhulumiwa.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar ,Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo,, Khamis Mbeto Khamis aliyewaonya wanasiasa akiwataka waache kuwatimbwisha wananchi.
Mbeto alisema si nia wala lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya Rais Dk Hussein Ali Mwinyi kumdhulumu mwananchi yeyote haki yake ya msingi.
Alisema CCM ina taarifa za kutosha kuwa baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka ACT Wazalendo,, wamekwenda huko Mangapwani na Bumbwini kinyume na taratibu kwa madai ya kusikiliza kero zinazohusu ardhi na fidia.
Aliongeza kusema kuwa pamoja na baadhi ya wananchi hadi sasa kutolipwa fidia zao, hiyo haihalalishi kuwa wameporwa au kudhulumiwa maeneo yao kinyume na sheria.
“Wanasiasa acheni kuchochea kuni za mitafaruku na kuigombanisha serikali. Tunaelewa kuna baadhi ya Wawakilishi wa ACT wazalendo wamefika Bumbwini na Mangapwani kuchochea mtafaruku huo wa ardhi “Alisema Mbeto akaongeza, katika maeneo yote ambayo serikali itakusudia kuyachukua kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kimaendeleo, watalipwa fidia na hatawapora haki zao.
“Inasikitisha kusikia Wawakilishi wa ACT wakitajwa kufika Bumbwini na Mangapwani kuchochea taharuki. Kamati ya Baraza la wawakilishi Zanzibar ndiyo yenye dhamana kwa idhini ya spika.”Alisema Mbeto.
“Rais Dk Mwinyi chini ya uongozi wa CCM hautamdhulumu haki mwananchi yeyote. Kilichofanywa na Wawakilishi hao ni kudandia jambo wasilolijua kwa nia ya kupata umaarufu usio na faida” aliongeza Mbeto.
