Chama cha Mapinduzi CCM kimeeleza kupokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mmoja wa waasisi na viongozi waandamizi nchini Mzee Cleopa David Msuya, kilichotokea leo Mei 07, 2025 Jijini Dar Es salaam.
“Mzee Msuya alikuwa miongoni mwa makada na viongozi waliotumikia Chama, Taifa letu na nchi yetu, kupitia nafasi alizoaminiwa kwa kuchaguliwa na kuteuliwa, kwa moyo wa dhati, uadilifu wa hali ya juu na uzalendo uaiotetereka.” Imesema taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Aidha kwaniaba ya @ccmtanzania Nchimbi ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na watanzania wote walioguswa na msiba huo mkubwa, akieleza kuwa wanaungana na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi hiki cha maombelezo ya siku saba alizotangaza rasmi leo kwa heshima za maisha na mchango wa Mzee Msuya kwa Tanzania.
CCM imeeleza kuwa Mzee Msuya ataendelea kukumbukwa kama Kiongozi aliyeacha alama za kudumu kwa Serikali na Chama Cha Mapinduzi.
