
Shilingi 35, 425,991,000 zimepitishwa na Bunge kuwa Bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Hata hivyo, Wizara hiyo inatarajiwa kukusanya Sh. 900, 000,000 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato kutoka taasisi zilizo chini yake.
Akiwasilisha Bungeni hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo jana Juni 6, 2022, jijini Dodoma, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amelithibitishia Bunge kuwa pamoja na mambo mengine Wizara hiyo imejizatiti kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuwahudumia Watanzania.
Waziri Mchengerwa amebainisha kuwa kati ya fedha hizo zilizotengwa kutekeleza majukumu ya wizara, Sh. Bilioni Sh.8, 201,882,000 zitakazotumika kwa mishahara ya watumishi, Sh. Bilioni 11,392,949,000 zitatumika kwa matumizi mengineyo na Bilioni 15,831,160,000 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo ipo chini ya wizara na taasisi zake.
Miradi mikubwa inayokwenda kutekelezwa na Wizara hiyo kwa mwaka 2022/23 ni ujenzi wa vituo vya mazoezi, kupumzika wananchi, Sports and Arts Arena ambayo itagharimia Sh.7,166,160,000, ujenzi wa eneo Changamani la michezo Dar es Salaam Sh.1,500,000,000, ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya michezo. Katika Shule Maalumu 56 za michezo Sh.2,000,000,000 na ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ambao utagharimu Sh.1,300,000,000 ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kwa lengo la kukuza na kuendeleza vipaji na kuendelea na ujenzi wa hostel ya wanafunzi.
