
Tanzania imepata Tuzo ya kuwa na banda bora lenye ubunifu wa kutangaza utalii katika maonesho ya 37 ya utalii ya Seoul International Travel Fair (SITF).
Hayo yamebainishwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea, Togolani Mavura baada ya kukabidhiwa Tuzo hiyo na Mwenyekiti wa Maandalizi ya maonesho ya SITF, Shin, Joong-mok.
Maonesho hayo yamefanyika katika jiji la Seoul, nchini Korea Kusini, kuanzia Juni 23 hadi 26, 2022.
“Tuzo hii ni ishara nzuri ya ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), na wadau wa utalii katika kuandaa ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya SITF.
“Tutaendelea kuzijongea fursa za kutangaza utalii wa Tanzania na kushiriki katika matukio mbalimbali yatakayofanyika hapa Korea.
Banda la Tanzania lilipambwa kwa kuonesha vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini ambapo picha za Utalii wa kiutamaduni, Mlima Kilimanjaro, fukwe za Zanzibar, nyumbu wanaovuka mto Mara, na madini ya Tanzanite zimewavutia wageni wengi waliotembelea maonesho hayo.
“Katika Banda la Tanzania wananchi wa Korea waliweza kujitokeza kwa wingi kunywa na kufurahia radha ya kahawa ya Tanzania.
“Tukio hili lilichangia Banda la Tanzania kutembelewa na wageni wengi.. Kahawa iliyotumika kwenye maonesho haya ni ile inayolimwa katika wilaya ya mbinga mkoani Ruvuma.
Aidha, wanawake wengi wa waliotembelea banda la Tanzania walivutiwa sana na ususi wa nywele ambapo walijitokeza kwa wingi kusuka nywele zao. Jambo ambalo walionesha kulifurahia sana.
Kwa upande wa Bodi ya Utalii Tanzania, ofisa habari na uhusiano, Augustina Makoye amesema “Tunaendelea kubuni njia mbalimbali za kutangaza utalii wa Tanzania ili vivutio vyetu viweze kujulikana zaidi katika soko hili ambalo wananchi wengi wameonesha kuvutiwa zaidi na vitu vya kiutamaduni,
Tutaendelea kuliwekea mkakati wa kutangaza utalii wa kiutamaduni kwa vitendo ili tuweze kuwavutia watalii wengi wa nchi ya Korea Kusini.
