
Ili bamia ioneshe mafanikio katika tiba ya mafua ni vema mgonjwa aitumie kwa kuzingatia maelekezo ya mtaalam wa tiba asilia.
Mtaalam wa Virutubisho Tiba, Abdallah Mandai, amesema ugonjwa wa mafua ambao unaathiri mirija ya kichwani kwenye mfumo wa kuvuta pumzi, bamia ni tiba anuwai ya tatizo hilo linalohusiana na kupumua.
Mandai ameyasema hayo leo Septemba 16, 2021 jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na kituo hiki kuhusu aina mbalimbali za tiba asili zinavyosaidia uponyaji wa watu wengi katika jamii.
Amesema mgonjwa wa mafua ajifushe gramu 100 za bamia lililokatwa katika vipande vidogovidogo na kuchemshwa muda wa dakika 10 likiwa limefunikwa vizuri kuzuia mvuke kupenya.
Amefafanua kuwa wakati wa kujifusha ni vema mgonjwa ajifunike kwa nguo nzito huku akivuta hewa ya mvuke huo katika kipindi cha dakika tatu hadi tano.
Baada ya maji hayo kupoa, mgonjwa ayanywe yote na kula bamia zote na kwamba azingatie kuwa tiba hiyo ni ya mara mbili kutwa muda wa siku tatu, mafua yatakuwa yamemtoka.
