
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolijia, Profesa Adolf Mkenda, amesema anaogopa watu wanaoridhika kwenye elimu kwa kudhani kuwa wamefika wakati bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha elimu inaboreshwa.
Prof. Mkenda alibainisha hayo jana Juni 13, 2022 wakati akifunga maonesho ya Elimu ya Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, jijini Dodoma.
Amesema kama elimu hapa nchini ni bora basi kusingekuwa na ulazima kwa baadhi ya kampuni kuajiri watu kutoka nje ya nchi, hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha elimu yetu inakidhi mahitaji yanayotakiwa katika soko la ajira.
“Lazima tukubali kuwa elimu yetu bado na inahitaji tuendelee kufanya kazi kwa nguvu sana ili kuiboresha kwa sababu ukweli ni kwamba kuna vyuo hadi sasa vinatoa wanafunzi ambao baada ya kumaliza mafunzo hawaajiriki kabisa kutokana na kutokuwa na ubora, hivyo ndugu zangu tusiridhike hatujafika kabisa,”amesema.
Pia amegusia jitihada ambazo serikali inaendelea kufanya ili kutafuta mikopo na benk ya NMB imekubali kutoa sh. bilion 200 kwa ajili ya kukopesha wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati na ufundi nchini.
“Mikopo hii haitakuwa kama ile inayotolewa na Bodi ya Mikopo kwa hiyo kama ni mfanyakazi atahitaji kumsomesha mtoto wake VETA atapewa mkopo huo kwa masharti nafuu,”amesema.
Profesa Mkenda amesema katika kuhakikisha mchakato wa kutoa mikopo katika ngazi hiyo linakuwa kwa ufasaha inahitajika kuwa na takwimu mahusus za vyuo vyote vinavyotoa mafunzo.
Kwa Upande wake Katibu Mtendaji wa NACTVET Dk. Adolf Rutayuga alisema katika kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa elimu ya mafunzo stadi yenye ubora zaidi, hadi kufikia Juni 2022 baraza lilikuwa limesajiri vyuo 454 vya elimu ya ufundi.
