Baba mmoja nchini Marekani amewaua kwa kuwapiga risasi watoto wanane, wakiwemo saba wa familia yake mwenyewe, katika tukio la kikatili lililotokea Jumapili asubuhi katika mtaa wa Shreveport.
Polisi wamesema shambulio hilo lilifanyika katika nyumba mbili tofauti na limeacha jamii ikiwa katika mshtuko mkubwa, likitajwa kuwa miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi ya mauaji ya halaiki katika miaka ya karibuni nchini humo.
Kwa mujibu wa polisi, watoto wote wanane waliuawa katika nyumba moja, wakiwa na umri kati ya miaka 3 hadi 11.
Wanawake wawili, akiwemo mke wa mshukiwa ambaye pia ni mama wa baadhi ya watoto hao, walijeruhiwa vibaya kwa risasi na kukimbizwa hospitalini.
Tukio hilo linaelezwa kuwa la kifamilia, huku sababu halisi ya shambulio hilo ikiwa bado inachunguzwa.
Mshukiwa wa tukio hilo ametajwa kuwa ni Shamar Elkins (31), ambaye alifariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi wakati akijaribu kutoroka.
Kabla ya tukio hilo, inaelezwa kuwa alifika katika nyumba moja na kumpiga risasi mwanamke mmoja kabla ya kuelekea nyumba ya pili ambako mauaji ya watoto yalifanyika.
Mtoto mmoja alikutwa amefariki juu ya paa akijaribu kukimbia, huku mwingine akiruka kutoka juu ya paa na kunusurika.
Taarifa kutoka kwa ndugu wa familia zinaeleza kuwa Elkins alikuwa katika mgogoro wa ndoa na mke wake, wakitarajiwa kufika mahakamani siku iliyofuata (leo Jumatatu) kwa ajili ya kupeana talaka.
Inadaiwa kulikuwa na mabishano makali kabla ya tukio hilo. Pia imebainika kuwa alikuwa na watoto na wanawake wawili tofauti, ambao wote waliishi karibu na eneo la tukio.
Mamlaka zimesema mshukiwa aliwahi kukamatwa mwaka 2019 kwa kosa la matumizi ya silaha na pia aliwahi kuhudumu katika Kikosi cha Taifa cha Walinzi wa Jeshi la Louisiana kwa miaka saba kabla ya kuondoka mwaka 2020.
Tukio hili limeibua hisia kali kwa viongozi na jamii, huku Mkuu wa Polisi wa Shreveport akieleza kushindwa kuelewa namna tukio la aina hiyo lingeweza kutokea.
