
Wanamgambo wa Al-Shabab wameshambulia kambi ya Muungano wa Afrika ambayo inahifadhi wanajeshi wa Burundi katikati mwa Somalia.
Idadi ya waliojeruhiwa bado haijabainika.
Hata hivyo, mashirika ya habari yanawanukuu mashuhuda wakisema kulikuwa na mapigano makali kwenye kambi hiyo, ambayo ni takriban kilomita 130 (maili 80) Kaskazini-mashariki mwa mji mkuu, Mogadishu.
“Magaidi walishambulia kambi ya jeshi la Burundi… kulikuwa na mapigano makali na hasara iliyotekelezwa pande zote mbili, lakini hatuna maelezo zaidi kuhusu tukio hili hadi sasa,” kamanda wa kijeshi wa eneo hilo Mohamed Ali aliliambia shirika la habari la AFP.
“Walianzisha shambulio hilo kwa mlipuko wa bomu kwenye gari kabla ya majibizano makali ya risasi kuzuka,” aliongeza.
Kikosi cha Muungano wa Afrika – ambacho sasa kinajulikana kama Atmis – kinajumuisha wanajeshi kutoka mataifa kadhaa ya Afrika: Uganda, Burundi, Djibouti, Kenya na Ethiopia.
Inaunga mkono Serikali ya Mogadishu katika mapambano yake dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab.
