
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Afrika Kusini ameuawa na mwingine kujeruhiwa katika shambulio la helikopta yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Monusco, umesema helikopta hiyo iliungua moto mchana wa jana Jumapili wakati ikielekea Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, ambako ilifanikiwa kutua.
Imesema mlinda amani mwingine alijeruhiwa katika shambulio hilo. “Monusco inalaani vikali shambulio hili la woga dhidi ya ndege yenye nembo ya Umoja wa Mataifa,” ilisema katika taarifa yake.
Jeshi la Ulinzi la Kitaifa la Afrika Kusini (SANDF) pia limethibitisha shambulio hilo. “Helikopta ya Oryx iliungua huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumapili Februari 5, 2023,” ilisema katika taarifa yake.
“SANDF iko katika harakati ya kuwafahamisha wanafamilia kuhusu wanajeshi waliohusika.”
