
Watu wapatao Sita wameuawa na vijiji kadhaa kuchomwa moto na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al Shabab katika mji wa pwani wa Lamu, nchini Kenya.
Polisi wamesema wapiganaji waliokuwa na silaha nzito walishambulia vijiji vya Widho eneo la majembeni Kaunti ya Lamu mapema leo Jumatatu.
Gazeti la The Star nchini Kenya limemnukuu Kamishna wa Kaunti ya Lamu Irungu Macharia aliyethibitisha kisa hicho akisema operesheni ya kuwasaka wavamizi hao inaendelea.
Hali ya taharuki imetanda katika eneo hilo huku doria za usalama zikiimarishwa.
Kundi hilo la wanamgambo limefanya mashambulizi mengi katika kaunti ya Lamu ambayo iko mpakani mwa Somalia- katika maeneo yanayofikiriwa kuwa ngome ya kundi hilo linaloshirikiana na mtandao wa Al Qaeda.
