Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema athari inayotokana na aina mpya ya kirusi cha Omicron bado iko juu baada ya idadi ya maambukizo ya virusi vya corona kuongezeka kwa asilimia 11 kote duniani wiki iliyopita.
Katika taarifa yake ya kila wiki kuhusu udhibiti na kuenea kwa virusi vya corona, WHO imesema kirusi cha Omicron kinahusika na ongezeko la kasi la virusi hivyo katika mataifa kadhaa ikiwa ni pamoja na yale ambayo tayari yalikuwa na udhibiti wa kirusi cha Delta.
WHO imeongeza kuwa ushahidi thabiti unaonesha kuwa kirusi cha Omicron kina ukuaji wa haraka zaidi kuliko kile cha Delta na uwezo wa kuongezeka mara mbili katika muda wa siku mbili hadi tatu huku ongezeko la maambukizi yakishuhudiwa katika mataifa kadhaa yanayojumuisha Uingereza na Marekani.
