
Mamia ya wanasiasa kutoka kote duniani wanatumia kampuni na benki za nje kuficha fedha zao.
Hayo ni kwa mujibu wa uchunguzi wa kina uliofanywa na muungano wa kimataifa wa vyombo vya habari wa ICIJ.
Uchunguzi huo uliopewa jina la Pandora Papers, ambao uliwahusisha waandishi habari 600 kutoka mashirika ya Washington, BBC, Guardian na DW, ulifanywa kutokana uvujishaji wa nyaraka takribani milioni 11.9 kutoka kampuni za huduma za kifedha kote duniani.
Data hizo zinabainisha shughuli za kampuni za wanasiasa zaidi ya 330 kutoka mataifa 91, wakiwemo wakuu 35 wa sasa na wa zamani wa mataifa na serikali, lakini pia wakiritimba, wahalifu na watu mashuhuri wanahusishwa.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mama yake wametajwa kwenye nyaraka hizo kuwa wanamiliki akaunti za siri Panama.
Aidha, ndugu zake watatu, wanamiliki kampuni tano za nje ya nchi zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 30. Kenyatta na familia yake hawakujibu maombi ya ICIJ ya kutoa maoni yao kuhusu taarifa hizo.
