
Serikali mkoani Dar es Salaam imewataka wananchi wake kuchukua tahadhari dhidi ya wimbi la tatu la mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Corona.
Mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla, ametoa tahadhari hiyo leo Dar es Salaam, wakati akiwahutubia wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Amefafanua kuwa tahadhari hiyo imezingatia mkoa wake kuwa na viashiria vya ugonjwa huo kutokana na kuwa ni lango kutoka na kuingia katika mikoa mingine na nchi jirani ambazo zina wimbi kubwa la maambukizi ya virus vya corona.
Makala ambaye alikuwa akizungumza huku akiwa amevalia barakoa, amesema tahadhari hiyo ni pamoja na wananchi wasipende kusogeleana, wazingatie kuvaa barakoa kwa usahihi, wanawe mikono na wafunike midomo wakati wa kukohoa na kupiga chafya.
Pia kwenye maeneo yenye msongamano kuwepo ndoo au miundombinu mingine ya maji tiririka ili kuwapa fursa watu mbalimbali kunawa mikono yao.
Aidha, Makalla amewaomba wananchi wa mkoa huo kwenda katika vituo vya afya punde wanapobaini homa kali au kushindwa kupumua kwani hakuna tatizo la uhaba wa vifaa tiba huku akiwataka kula mlo kamili na kufanya mazoezi ya viungo kila siku.
